LONDON, England
KOCHA wa Inter Milan, Rafael Benitez ametuliza mzuka wa mashabiki wa klabu hiyo akidai hali ni shwari tangu alipochukuwa nafasi ya Jose Mourinho aliyetimkia Real Madrid.
Benitez alisema hali ya ndani ya kikosi hicho ni shwari na wachezaji wana furaha licha ya kuibuka taarifa ana hali ngumu kutokana na kushindwa kuipiku rekodi ya mafanikio ya Mourinho aliopata muda mfupi baada ya kutua San Siro.
"Hapana siwezi kusema kuna matatizo makubwa katika timu, wachezaji wanafanya kazi nzuri lakini pia ni kweli kuna changamoto zake wakiwemo wachezaji wengi tegemeo ambao ni majeruhi" alisema Benitez.
Mashabiki wa klabu hiyo walimshambulia kwa maneno makali Benitez baada ya Inter Milan kuchapwa mabao 3-1 na Tottenham Hotspurs katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kulazimishwa sare na Brescia katika mechi ya ligi.
Benitez aliwapoza mashabiki kwa kuahidi mambo yatakuwa mazuri ifikapo Januari, mwakani kwa madai hivi sasa anakabiliwa na hali ngumu kutokana na kuandamwa na majeruhi wengi wa kikosi cha kwanza.
"Tutakuwa katika nafasi nzuri ikifikapo Januari, tutaangalia pia mchakato wa usajili ili kuongeza nguvu. Tunaweza kufanya kitu baada ya kuumia Walter (Samuel)," alidokeza Benitez.
Inter Milan inakabiliwa na idadi kubwa ya majeruhi akiwemo kipa Julio Cesar, Douglas Maicon, Thiago Motta, Esteban Cambiaso, Wesley Sneijder na Walter Samuel atakayekuwa nje ya uwanja miezi sita baada ya kuumia uvungu wa goti.
No comments:
Post a Comment