MADRID, Hispania
TIMU ya soka ya Real Madrid itamkosa kocha wake Jose Mourinho katika michezo miwili ijayo baada ya kocha huyo kufungiwa na Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF).
Kocha huyo wa zamani wa Inter Milan amefungiwa kutokana na utovu wa nidhamu aliouonyesha kwa mwamuzi Jose Luis Paradas Romero katika mchezo baina yao na timu ya Murcia ambao timu hiyo ilishinda mabao 5-1 katika michuano ya Copa del Rey.
RFEF hawakufurahishwa na tabia ya Mourinho aliyoonyesha kwa mwamuzi huyo hivyo kuamua kumfungia kocha huyo kwa mechi mbili.
"Amesimamishwa kwa kumtolea lugha isiyofaa mwamuzi kitendo ambacho hakikubaliki kimichezo," ilisema taarifa ilichapishwa kwenye mtandao wa klabu.
Mourinho atakosa mechi za mwishoni mwa wiki dhidi ya Sporting Gijon na mchezo wa nyumbani dhidi ya Athletic Bilbao Novemba 23 kutokana na kufungiwa huko.
No comments:
Post a Comment