MABAO ya dakika za mwisho yaliyofungwa na wachezaji wa Simba Jerry santo na Emmanuel Okwi yaliihakikishia mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Majimaji ya Ruvuma na kumaliza raundi ya kwanza ya ligi hiyo wakiwa wanaongoza.
Yanga ambao wanalifukuzia taji hilo pia waliwafunga Toto Africa ya Mwanza na kuweka matumaini hai ya kunyakua taji hilo, ambalo liliwaponyoka msimu uliopita. Bao la Nurdini Bakari liliihakikishia ushindi timu hiyo ambayo imekuwa ikitoa suluhu katika michezo yake miwili iliyopita iliyowafanya wapinzani wake kuwapita na kuchukua usukani kuongoza ligi.
Katika michezo ya Jumapili pia ilishuhudia matajiri wa mjini, Azam FC, wakipeleka ujumbe wa kuogopwa baada ya kuifunga Ruvu Shooting mabao 4-1 ambapo Mrisho Ngassa alipiga mabao matatu peke yake.
Katika michezo mingine, Polisi Dodoma waligawana pointi na JKT Ruvu katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. na kwa matokeo hayo Simba na Yanga wamelinda nafasi zao ya kwanza na ya pili kwa pointi 27 na 25, wakati Azam imepaa hadi nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 20, juu ya Mtibwa ambayo imeanguka nafai moja.
No comments:
Post a Comment