LONDON, England
KIKUNDI cha Kimataifa cha kutetea haki za mashoga kimemtaka Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Sepp Blatter kuwaomba radhi kufuatia kauli yake aliyoitoa hivi karibuni kuhusiana na mashoga watakaosafiri kwenda Qatar kushuhudia fainali za Kombe la Dunia 2022.
Blatter alizungumza Jumatatu kuwa mashabiki ambao ni mashoga "inabidi wajizuie kufanya mambo yao ya kishoga" wakati wa Kombe la Dunia Qatar, ambapo huko vitendo vya kishoga ni haramu.
Mkurugenzi wa mawasiliano wa tawi la Ulaya la kikundi hicho Juris Lavrikovs, alisema kauli hiyo imewashangaza na imewakwaza sana.
"Nafikiri wangetoa ripoti kamili inayoeleweka na sio kuzungumza juu juu," alisema Lavrikovs akiwaambia waandishi wa habari. "Tunaongelea suala la haki za msingi za binadamu ambayo inakiukwa."
Blatter alitoa kauli hiyo Jumatatu Afrika Kusini wakati wa chakula cha mchana. aliulizwa kama naona kutakuwa na tatizo lolote la kiutamaduni wakati mashindano hayo yatapofanyika Qatar.
"Naweza kusema inabidi wajizuie kufanya vitendo vyao vya kishoga wakati wakiwa huko," alisema Blatter huku akitabasamu.
"Huu si utani ni suala la kufa na kupona," alisema Lavrikovs. "Qatar na zaidi ya nchi 70 duniani bado wanapingana na masuala ya ushoga na nchi zingine zinafikia hatua ya kumnyonga yoyote atakayebainika anafanya vitendo hivyo.
"Inasikitisha kuona taasisi ambayo inasimamia michezo, na huwa inapingana na aina yoyote ya ukandamizaji, ikitoa kauli kama hiyo." alimalizia Lavrikovs.
No comments:
Post a Comment