Monday, February 28, 2011

UJERUMANI KUINGIZA TIMU TANO MICHUANO YA CHAMPIONS LEAGUE MSIMU UJAO.

MUNICH, German
CHAMA cha Soka nchini Ujerumani (DFB) msimu ujao kitaingiza timu nne kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, kufuatia nchi hiyo kupanda katika viwango vya soka barani Ulaya mbavyo hutolewa kila mwezi na Shirikisho la Soka barani humo (UEFA) kwa vigezo vya michuano iliyo chini ya UEFA.

Ujerumani wamefikia hatua hiyo baada ya kukamata nafasi ya tatu kwenye viwango vya ubora barani Ulaya sifa ambayo inaifanya nchi hiyo kutoa fursa kwa mshindi wa kwanza wa pili na watatu wa ligi kuingia moja kwa moja katika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Ulaya huku mshindi wa nne akianzia katika hatua ya mtoano.

Mshindi wa tano na wa sita katika ligi ya Ujerumani pia watacheza moja kwa moja katika hatua ya makundi la michuano ya ligi ya barani Ulaya ambayo huzishirikisha klabu 64 toka msimu uliopita baada ya utaratibu wa uendeshaji wa michuano hiyo kubadilishwa.

Sababu ya Ujerumani kuingia katika utaratibu huo na kushika nafasi ya tatu katika viwango vya ubora wa soka barani ulaya, ni kufutia ushindi wa klabu za nchi hiyo uliopatikana juma hili ambapo Bayern Munich walifanikiwa kuwachapa Inter Milan bao moja kwa sifuri, Schalke 04 nao wakalazimisha sare ya bao moja kwa moja na Valencia katika mchezo wa ligi ya mabingwa huku Bayer Leverkusen wakifanikiwa kuiondosha Metalist Kharkiv ya nchini Ukraine kwenye michuano ya ligi ya barani ulaya na VfB Stuttgart wakabamizwa na Benfica toka nchini ureno.

Mtendaji mkuu wa DFB Reinhard Rauball amesema wamefurahishwa na hatua hiyo na sasa wanachokitazama mbele ni kukwea zaidi kutoka katika nafasi ya tatu hadi nafasi ya pili na ikiwezekana kuikamata nafasi ya kwanza.

Wakati Ujerumani wakishika nafasi ya tatu, nchi ya Italia yenyewe imeporomoka nafasi moja chini kutoka nafasi ya tatu hadi ya nne kwenye viwango vya ubora duniani, ambapo sasa nchi hiyo itawakilishwa na klabu tatu kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Sababu ya kuporomoka ni kupoteza kwa vilabu vya nchi hiyo katika michuano ya kimataifa ambapo Inter Milan walikubali kisago cha bao moja kwa sifuri kutoka kwa Bayern Munich, Ac Milan nayo ilipoteza kwa Tottenham Hotspurs kwa kukubalia kichapo cha bao moja kwa sifuri huku AS Roma wakachapwa mabao manne kwa matatu Shakhtar Donetsk.

Kama itakumbukwa vyema pia klabu ya Sampdoria ilitolewa na Werder Bremen ya nchini ujerumani katika hatua ya mtoano ili hali katika michuano ya ligi ya barani ulaya klabu ya Napoli, imetolewa baada ya kutandiskwa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Villarreal ya nchini Hispania.

Hii inakua ni mara ya kwanza kwa nchi ya Italia kuporomoka kwa viwango vya ubora wa soka barani ulaya baada ya miaka 12 kupita ambapo kwa mara ya mwisho Italia waliingia katika nchi tatu bora zinazofanya vyema mwaka 1999 kufuatia vilabu vya soka vya nchini humo kutwaa vikombe 13 vya barani ulaya kuanzia mwaka 1990.

No comments:

Post a Comment