KIUNGO wa klabu ya Chelsea ya nchini Uingereza Michael Essien amesema atakua miongoni mwa mashabiki watakaohudhuria kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya timu ya taifa ya Ghana dhidi ya timu ya taifa ya Uingereza utakaochezwa leo katika Uwanja wa Wembley, London.
Essien ametangaza dhamira hiyo huku akitanabaisha wazi kwamba yeye ni shabiki wa timu ya taifa lake hivyo hatosita kuelekea uwanjani kuungana na mashabiki wengine wa timu ya taifa ya Ghana ambayo ilishindwa kuandika historia ya kutinga kwenye hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2010 baada ya kutolewa na timu ya taifa ya Uruguay katika hatua ya robo fainali.
Alisema hana budi kufanya hivyo na katu hana ubaya na yoyote ndani ya timu ya taifa ya Ghana pamoja na viongozi wa GFA kufuatia maamuzi aliyoyachukua ya kukaa pembeni kwa muda kabla ya kurejea kikosini kujiunga na wengine ndani ya Black Stars.
Hata hivyo Essien ametoa sababu za kuchukua maamuzi ya kujiweka pembeni ambapo alisema kipindi hiki anakitumia kama sehemu ya kuupumzisha mwili wake baada ya kuumia magoti yote mawili akiwa na timu ya taifa ya Ghana ambayo aliiwezesha kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2010.
Ghana wanaingia uwanjani hiyo kesho huku wakiwa na kumbu kumbu nzuri ya kushinda mchezo wao wa kufuzu kucheza fainali za mataifa ya bara la Afrika za mwaka 2012 kwa kuifunga timu ya taifa ya Congo Brazzaville mabao matatu kwa sifuri.
No comments:
Post a Comment