KLABU ya Manchester City imeonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo wa Real Madrid Kaka kwa mujibu wa gazeti nchini Uingereza.
Man City wamepania kuongeza nguvu nafasi ya kiungo mchezeshaji katika kikosi chake kwenye kipindi cha usajili majira ya kiangazi, na wameona kwamba Kaka (28) ndio chaguo lao muafaka.
Kaka alijiunga na Real Madrid akitokea AC Milan mwaka 2009, lakini mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil ameshindwa kuonyesha cheche zake akiwa Santiago Bernabeu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.
Toka amepona amekuwa akisugua benchi, na chaguo la Kocha wa Madrid Jose Mourinho limeonekana kuangukia zaidi kwa viungo washambuliaji Mesut Oezil na Angel Di Maria.
Kwa hali inayomkabili hapo Madrid mchezaji huyo kuna uwezekano mkubwa wa kuondoka katika timu hiyo katika majira ya kiangazi, ambapo tayari Chelsea wameonekana kummezea mate mchezaji huyo, lakini Man City wanaamini watamnyakua mchezaji huyo.
Matajiri wa Urusi timu ya Rubin Kazan nao pia wanatamani kupata saini ya mchezaji huyo, lakini Kaka anaonekana kuvutiwa zaidi na timu za Uingereza.
No comments:
Post a Comment