Wednesday, March 16, 2011

RONALDO DE LIMA KUWA WAKALA WA WACHEZAJI.

RIO DE JENEIRO, Brazil
KWASASA mchezaji nguli kutoka Brazil Ronaldo ameonyesha nia yake ya kuhamia kwenye uwakala mara baada ya kutundika daruga kwa kuwawakilisha vijana chipukizi wa Brazil, ambapo anatarajia kuanza kazi hiyo ya uwakala kwa kuwachukua wachezaji chipukizi wa nchi hiyo Lucas na Neymar kama wateja wake wa kwanza.

Neymar anayechezea klabu ya Santos nchini humo na Lucas anayechezea Sao Paulo ndio chipukizi wanaowindwa na klabu nyingi kwa sasa, na wachezaji hao ndio walisaidia kwa kiasi kikubwa Brazil kunyakuwa Ubingwa wa Amerika Kusini wa vijana chini ya miaka 20 na kukata tiketi ya kucheza michuano ya Olympic.

Nyota huyo wa zamani wa klabu za Barcelona, Real Madrid, Ac Milan na Inter anajua matatizo wanayokutana nayo wachezaji chipukizi katika soko la kuuza wachezaji, na anaamini kwa kuingia huko katika shughuli hiyo anaweza kuwalinda.

"Kuna wanamichezo wengi wazuri hapa Brazil wanayohitaji huduma kama hii. Kwa kuanzia hatuwezi kuwahudumia wote na tutawahudumia wachache. Neymar na Lucas wametuvutia, kwasababu ndio watakuwa tegemeo la timu ya Brazil kwa baadae na watacheza Kombe la Dunia 2014," Alisema Ronaldo akiwaambia waandishi wa habari kuhusu nia yake hiyo.

Mchezaji huyo ambaye amewahi kuchukua Kombe la Dunia mara mbili akiwa na timu ya Brazil tayari ameanza mazungumzo na baba yake Lucas pamoja na wakala wa Neymar kuhusu suala la kuwawakilisha wachezaji hao.

No comments:

Post a Comment