Tuesday, March 1, 2011

ROONEY AKWEPA KITANZI.

LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Manchester United Wayne Rooney ameepuka adhabu ambayo huenda ingemuangukia kutoka ndani ya Chama cha Soka nchini humo (FA) kufuatia kumpiga kiwiko kiungo wa klabu ya Wigan Atheletic James McCarthy, pindi klabu hizo zilipokutana mwishoni mwa juma lililopita.

Mshambuliaji huyo ameepuka adhabu hiyo kutokana na kitendo hicho kuainishwa kwenye taarifa ya muamuzi Mark Clattenburg ambapo amekielezea kama ajali ambayo ilijitokeza katika mchezo huo uliomalizika kwa Man Utd kuibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Muamuzi huyo amekiorodhesha kitendo hicho katika taarifa yake sambamba na kukitolea maelezo kupitia vyombo vya habari ambapo amekiri alimuona Rooney akifanya kitendo hicho lakini amebainisha kwamba haikua kusudio lake bali kilitokea wakati akiwa kwenye harakati za kuwania mpira wa kiungo huyo wa Wigan.

Shinikizo la mshambuliaji huyo kuadhibiwa na FA lilitolewa na meneja wa klabu ya Wigan Roberto Martinez mara baada ya mtanange huo kumalizika huko DW Stadium ambapo alieleza kwamba muamuzi Mark Clattenburg alistahili kumuonyesha kadi nyekundu Wayne Rooney kufuatia kosa alilomfanyia James McCarthy.

Endapo Wayne Rooney angekumbwa na adhabu hiyo ingemlazimu kuwa nje kwa takriban michezo mitatu ambapo angeanza na mchezo wa kesho dhidi ya Chelsea kisha akafuata mchezo dhidi ya Liverpool na mwisho wa adhabu yake ingeangukia katika mchezo wa kombe la FA ambapo Man utd watakutana na mshindi wa mchezo kati ya Arsenal dhidi ya Leyton Orient.

No comments:

Post a Comment