Monday, March 28, 2011

SAHA AHOFIA KUSHINDWA KUMALIZIA MSIMU HUU.

LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa kimataifa toka nchini Ufaransa na klabu ya Everton Louis Saha amesema hadhani kama atarejea tena uwanjani msimu huu kufuatia maumivu ya kifundo cha mguu aliyoyapata mwishoni mwa juma lililopita.

Saha ametoa mtazamo huo huku klabu yake ikionyesha nia ya kutaka kumuona anarejea tena uwanjani kuisaidia katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu.

Alisema alijisikia maumivu makali sana baada ya kuumia kifundo cha mguu akiwa kwenye mchezo wa ligi mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Fulham na mpaka sasa hali yake bado haitabiriki hivyo hadhani kama anaweza kuuwahi muda wa ligi uliosalia.

Hatua hiyo pia inaonekana kumpa wakati mgumu meneja wa klabu ya Everton David Moyes hasa ikizingatiwa kikosi chake kwa sasa kinaendelea kuwakosa wachezaji muhimu kama Saha pamoja na wachezaji wengine waliopo kwenye benchi la majeruhi.

Alipojiwa juu ya matarajio yake kwa mchezaji huyo Moyes alishindwa kuthibitisha lolote zaidi ya kusema anasubiri taarifa za majibu kutoka kwa daktari ambazo zitaainisha Saha atakuwa nje kwa muda gani.

Kikosi cha klabu ya Everton kwa sasa kinashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza na endapo kitaendelea kupanda zaidi ya hapo huenda kikapata nafasi ya kucheza michuano ya barani ulaya msimu ujao.

No comments:

Post a Comment