Friday, April 29, 2011

BARCELONA YAFIKIRIA KUMSHTAKI MOURINHO.

BARCELONA, Hispania
UONGOZI wa klabu ya FC Barcelona unajipanga kumshitaki meneja wa klabu ya Real Madrid José  Mourinho kufuatia maneno yake makali aliyoyatoa mbele ya vyombo vya habari mara baada ya mchezo wa usiku wa kuamkia hii leo kumalizika huko Estadio Stantiago Bernabeu.

Uongozi wa klabu hiyo unafikiria hatua hiyo baada ya kukiri kuchomwa na maneno makali ambayo wamedai hayapaswi kuzungumza na mtu kama Mourinho aliedumu katika ramani ya soka kwa vigezo vyenye sifa kubwa duniani.

Katika mkutano na waandishi wa habari Mourinho alionyeshwa kuchukizwa na namna ya matokeo ya mchezo wa jana yalivyopatikana ambapo alifikia hatua ya kudai kwamba ni vigumu kwa upande wake kupata ushindi anapocheza na klabu ya Barcelona.

Alisema hafahamu kama klabu hiyo inajidaia jina la UNICEF lililopo katika jezi zao ambapo ameeleza wazi kwamba huenda jina hilo linafanyiwa tangazo kwa namna yoyote ile kwa kuhakikisha wanashinda ili ujumbe ufike kwa wahusika salama wa salamini.

Pia Mourinho akaendelea kuishambulia klabu hiyo kwa kueleza kwamba huenda ukaharibu uliopo kati yao na Rais wa Shirikisho la Soka nchini Hispania Angel Maria ambae pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) ukawa unachangia kwa klabu hiyo ya Catalan kupata ushindi kirahisi.

Hata hivyo ameomba aelezwe wazi kwamba kulikua na uhalali gani kwa Pepe kuonyweshwa kadi nyekundu na muamuzi Wolfgang Stark kutoka nchini Ujerumani ili hali tayari ilikua imeshaonekana wazi kwamba mchezaji huyo pamoja na Daniel Alves walikua katika harakati za kuuwani mpira.

Pia akahoji adhabu aliyopewa ya kuondolewa kwenye benchi na kutakiwa kukaa jukwaani ili hali alikua akitetea maslahi ya kikosi chake lakini akaendelea kuuliza kwa nini beki wake Sergio Ramos alionyeshwa kadi ya njano ambayo inamfanya aukose mchezo wa merejeano utakaochezwa Camp Nou juma lijalo.

Katika hatua nyingine Mourinho akamgeukiwa kocha wa Barcelona Pep Guardiola Isala kwa kumsifia kuwa ni kocha mzuri lakini amekua akichafuliwa na sifa ya kutwaa ubingwa wa barani Ulaya kwa kashfa za kikosi chake kupendelewa katika michezo muhimu.


Akitolea mfano wa mwaka 2009 meneja huyo wa kimataifa toka nchini Ureno ametanabaisha kwamba katika mwaka huo, Barcelona walibebwa wazi wazi na muamuzi kutoka nchini Norway Tom Ovrebo ambae aliwanyima Chelsea haki ya kutinga hatua ya fainali kufautia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja yaliyopatikana katika mchezo huo.

Alisema mara baada ya mchezo huo wachezaji wa Chelsea wakiongozwa na Didier Drogba walimlalamikia muamuzi huyo kutokana na maamuzi mabovu aliyoyatoa dhidi yao lakini mshambuliaji huyo alijikuta akiambulia adhabu huku Barcelona wakisonga mbele katika hatua ya fainali na kufanikiwa kutwaa ubingwa mbele ya Man Utd.

Lakini pamoja na kusema yote hayo Jose Mourinho akaendelea kutamba kikosi chake huku akisema kwamba wao ndio vinara wa kutwaa ubingwa wa barani Ulaya hivyo watakwenda mjini Barcelona kushindana na anaamini nafasi yao ya kusonga mbele bado ipo.


Guardiola alipozungumza na waandishi wa habari hakugusia lolote juu ya tuhuma hizo zaidi ya kusifia ushindi uliopatikana ugenini ambao anaamini ulichangiwa na changamoto ya wachezaji vijana kumi na mbili aliosafiri nao toka mjini Barcelona hadi mjini Madrid.

No comments:

Post a Comment