Saturday, April 23, 2011

RAMOS ALIDONDOSHA KOMBE LA MFALME.

MADRID, Hispania
KUFUATIA furaha iliyopitiliza beki wa pembeni wa klabu ya Real Madrid Sergio Ramos alijikuta akiangusha kombe la ubingwa wa michuano ya Mfalme ambayo jana ilifikia tamati mjini Valencia kwa The Merengues kuibuka kidedea dhidi ya mabingwa wa soka nchini Hispania Fc Barcelona.

Sergio Ramos alijikuta akiangusha kombe la ubingwa wa michuano hiyo wakati kikosi cha Real Madrid kilipokua kikipita katika mitaa ya mji wa Valencia kikiwa juu ya gari maalum ambalo huwawezesha mashabiki kuwaona wachezaji kiurahisi.

Hata hivyo imeelezwa kwamba kombe hilo lenye uzito wa kilogram nane na urefu wa sentimita 78 limeripotiwa kuwa katika hali ya usalama licha kuingia sehemu ya chini ya gari walilokua wamepanda wachezaji.

Real Madrid wametawazwa kuwa mabingwa wa kombe la Mfalme baada ya miaka 18 iliyopita kufuatia ushindi wa bao moja kwa sifuri lililofungwa na Cristiano Ronaldo katika dakika ya 103.

José Mourinho alieweka historia ya kutwaa ubingwa wa kombe la Mfalme ambao pia ni ubingwa wake wa kwanza toka alipojiunga na klabu hiyo ya Stantiago Bernabeu alisema haikuwa kazi rahisi kukamilisha shughuli ya ushindi walioupata lakini kikubwa amefurahishwa na mafanikio yaliyopatikana.

Alisema hatua inayomfariji ni kumaliza mchezo huo akiwa na mawazo chanya ambayo ana hakika yatamsaidia katika mchezo ujao ambao utamkutanisha na Barcelona kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

No comments:

Post a Comment