Saturday, April 23, 2011

ZAMALEK WALA KIBANO CHA CAF.

CAIRO, Misri
MABINGWA wa soka nchini Misri Zamalek FC sasa watalazimika kucheza michezi miwili ya kimataifa iliyo chini ya Shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) bila ya kuwa na mashabiki uwanjani pamoja na kulipa faini ya dola za kimarekani 80,000.

Maamuzi ya klabu hiyo kongwe barani Afrika ya kucheza bila ya kuwa na mashabiki katika uwanja wa nyumbani yamefikiwa katika mkutano wa Kamati ya Nidhamu CAF kwa ajili ya kupitia matatizo ya kinidhamu yaliyojitokeza kwenye michuano ya kimataifa barani humo.

Zamalek wamefikwa na dhoruba hilo baada ya mashabiki wake kuingia uwanjani wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya mabingwa wa nchini Tunisia Club Africain uliochezwa mapema mwezi wa tatu.

Club Africain pia wametozwa faini ya dola za kimarekani 10,000 kufuatia kosa la baadhi ya mashabiki wao kuingia uwanjani wakati wa mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Tunisia dhidi ya Zamalek.

Kamati ya nidhamu ya CAF pia aimewaadhibu mabingwa wa zamani wa barani Afrika Enyimba ya nchini Nigeria kwa kuwatoza faini ya dola za kimarekani 20,000 kufuatia malumbano yaliyojitokeza kati ya wachezaji wa klabu hiyo dhidi ya klabu ya US Bitam ya nchini Gabon hali ambayo ilipelekea askari polisi kuingia katika sehemu yua kuchezea.

Enyimba pia wamepewa onyo kali na kamati hiyo ya nidhamu na endapo watashindwa kutii amri hiyo huenda wakafungiwa kucheza katika uwanjani wao wa nyumbani wa uliopo mjini Aba.

Klabu ya Mouloudia Alger ya nchini Algeria nayo imetozwa faini ya dola za kimarekani 5,000 kufuati mashabiki kuingia uwanjani wakati wa mchezo wa kombe la shirikisho dhidi ya Dynamos ya nchini Zimbabwe pamoja na klabu ya AS Aviacao ya nchini Angola nayo imeguswa na faini hiyo.

Klabu ya Deportivo Maxaquene, ya nchini Msumbiji, Kano Pillars ya nchini Nigeria pamoja na As Vita ya jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo zote kwa pamoja zimetozwa faini ya dola za kimarekani 5000 kwa kosa la mashabiki kuingia uwanjani.

Shirikisho la soka nchini Senegal nalo limeangukiwa na adhabu ya kutakiwa kulipa faini ya dola za kimarekani 5,000 kufuatia mashabiki kuingia uwanjani mara baada ya mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya bara la Afrika kumalizika kati ya timu ya taifa ya nchi hiyo dhidi ya Cameroon walioibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri.

No comments:

Post a Comment