Saturday, April 23, 2011

WENGER AWAJIA JUU WAANDISHI WA HABARI.

LONDON, England
KOCHA wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger amelaani kitendo cha baadhi ya waandishi wa habari kukuza maneno yanayo zungumzwa juu ya klabu hiyo ya kaskazini mwa jiji la London ambayo ipo katika harakati za kutaka kumaliza ukame wa kutwaa vikombe kwa kipindi cha miaka sita sasa.

Wenger amelaani kitendo hicho kufuatia moja ya vyombo vya habari nchini Hispania kuripoti kwamba nahodha na kiungo wa klabu ya Arsenal Cesc Fabregas alizungumza kauli inayoenda kinyume na sera za mzee huyo wa kifaransa mapema jana kabla ya mchezo wa ligi ya Uingereza dhidi ya Tottenham Hotspurs.

Alisema kila mmoja ana uhuru wa kuzungumza na kuandika la kwake lakini isizidi uwezo wa kuikandamiza Arsenal kwa utashi wa mtu ama watu binafsi kwa kupitia mianya ya wachezaji wake ambao amekiri anawatambua tabia zao.

Katika chombo hicho cha habari Cesc Fabregas alinukuliwa akisema kwamba ni wakati wa klabu ya Arsenal kufikiria kutwaa vikombe la kuachana na kasumba ya kukuza vijana, taarifa ambayo Arsene Wenger amedai haiingii akilini kama imesemwa na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23.

Katika hatua nyingine Arsene Wenger ameendelea kusisitiza jambo la kuhakikisha anapigana hadi tone la mwisho katika harakati za kusaka ubingwa msimu huu licha ya matokeo ya sare ya mabao matatu kwa matatu yaliyopatikana jana huko White Hart Lane.

Alisema ubingwa bado upo wazi na haoni sababu ya kukiondoa kikosi chake katika harakati za kuuwani ubingwa ambao kwa sasa unawaniwa na klabu yake, Man Utd pamoja na Chelsea ambao wanakamata nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao dhidi ya washika bunduki wa Ashburton Grove.

Alisema katika mchezo wa jana asilimia kubwa ya wachezaji wake walishindwa kwenda sambamba katika kipindi cha pili hali ambayo ilipelekea Spurs kusawazisha bao la tatu kupitia mkwaju wa penati.

Nae meneja wa klabu ya Tottenham Hotspurs Harry Redknapp amesema kuiujumla wachezaji wake walicheza kwa kujituma tena bila kuvunjika moyo baada ya kuwa nyuma kwa idadi ya mabao matatu na kwa bahati nzuri juhudi zao binafsi ziliwaokoa kujinusuru nyumbani.

Hata hivyo amedai kwamba Arsenal walicheza vizuri sana katika kipindi cha kwanza hatua ambayo ilipelekea kupata mabao matatu ya kuongoza.

No comments:

Post a Comment