Tuesday, May 3, 2011

BAFANA BAFANA KUTUA NCHINI MEI 12.

DAR ES SALAAM, Tanzania
KIKOSI kamili cha timu ya Taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana) kinatarajiwa kutua nchini mei 12 mwaka huu kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars mchezo utakaochezwa Mei 14 katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura kikosi cha Bafana bafana kinatarajiwa kushuka na nyota wake wote isipokuwa kiungo wake tegemeo Steven Pienaar anayechezea klabu ya Tottenham Hotspurs ya Uingereza.

Mchezo huo ni mahsusi kwa ajili ya timu hizo kujiandaa na mechi zao ngumu ugenini za kusaka tiketi ya kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (CAN) itakayofanyika Equatorial Guinea na Gabon 2012.

Stars inajiandaa na mchezo dhidi ya Afrika ya Kati utakaochezwa huko Bangui nchini humo June 4 wakati Bafana Bafana watakuwa Cairo, Misri kuikabili timu ya Taifa ya nchi hiyo "The Pharaohs".

Stars inatarajiwa kujipa kambini Mei 7 mwaka huu kujiandaa na mchezo huo huku TFF ikiwa tayari imewaombea ruhusa wachezaji wa Stars waliopo nje ya nchi kurudi kuja kuongeza nguvu kwa ajili ya mchezo huo.

Wachezaji walioombewa ruhusa kuja kujiunga na wenzao na wanazotoka katika mabano ni pamoja na Idrissa Rajabu (Sofa paka, kenya), Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Dan Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada), na Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden).

No comments:

Post a Comment