Tuesday, May 3, 2011

FERGUSON AWATUPIA LAWAMA WAAMUZI KUFUATIA KUFUNGWA KWAO.

LONDON, England
KOCHA wa Manchester United Sir Alex Ferguson ameendelea na kasumba yake ya kuwalaumu waamuzi wanaochezesha michezo ambayo humalizika vibaya kwa kikosi chake kupoteza ambapo mara hii amemuangushia lawama muamuzi wa mchezo wa jana Chris Foy kwa kusema aliwanyonya kwa kushindwa kuwapa mkwaju wa penati.

Sir Alex Ferguson alisema muamuzi Chris Foy hakustahili kuwanyima penati ambayo ilionekana dhahiri baada ya mshambuliaji wake kuchezewa rafu na beki wa kushoto wa klabu ya Arsenal Gael Clich.

Hata hivyo amekiri kwamba matokeo hayo yamewapa wakati mgumu wa kurejea katika ushindani wa kutwaa ubingwa kufuatia tofauti ya point tatu iliopo kati yao na Chelsea ambao walikua hawapewi nafasi ya kutetea taji lao baada ya kupoteza point kadhaa miezi iliyopita.

Alisema kwa bahati nzuri mchezo unaofuata unawakutanisha na Chelsea na anaamini mchezo huo ndio utakaoamua nani atajitengenezea mazingira ya kutwaa ubingwa msimu huu lakini pia akazungumzia suala la kucheza nyumbani huko Old Trafford ambapo yeye anaamini hiyo ni faida kubwa sana kwao.

Kocha wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger hakusita kukisifia kikosi chake kwa soka safi walilolionyesha katika mchezo huo wa jana lakini pia anaamini ushindi wa bao moja kwa sifuri uliopatikana utawaongezea chachu ya kusaka mafanikio katika michezo iliyobaki.

Bao pekee lililoipa ushindi Arsenal katika mchezo huo wa jana liliwekwa kimiani na kiungo wa kimataifa toka nchini Wales Aaron Ramsey katika dakika ya 55 ambapo bao hilo linampa nafasi ya kuandika historia ya kupachika bao la kwanza toka alipovunjika mguu miezi 14 iliyopita.

Alipohojiwa na waandishi wa habari Aaron Ramsey alisema alikua hafamu kama atapewa nafasi ya kuanzishwa katika kikosi cha kwanza lakini mapema jana Wenger alimuarifu juu ya kumpa nafasi kufuatia nahodha na kiungo Cesc Fabregas kupata maumivu ya nyama za paja.

No comments:

Post a Comment