Wednesday, June 22, 2011

ZWANZIGER AKEMEA MALUMBANO YA LOEW NA BALLACK.

MUNICH, Ujerumani
RAIS wa Shirikisho la Soka nchini Ujerumani Theo Zwanziger amelaani malumbano yanayoendelea kati ya Kocha Mkuu wa timu ya taifa Joachim Loew dhidi ya kiungo wa klabu ya Bayern Liverkusen Michael Ballack.

Zwanziger alisema malumbano yanayoendelea kati ya watu hao wawili hayamfurahishi na angependa yakome mara moja kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wadau wa soka nchini Ujerumani kusikia suala jipya linalohusiana na soka lao.

Alisema endapo hali hiyo itaendelea kuna kila sababu ya kuleta mpasuko kwa mashabiki hatua ambayo sio nzuri kufautia mchezo huo kutumika kama sehemu ya kudumisha urafiki na kuendeleza undugu.


Malumbano kati ya kocha Loew dhidi ya Ballack yaliibuka mara baada ya kocha huyo kuzungumza na vyombo vya habari juma lililopita ambapo alieleza wazi kwamba kiungo huyo ana nafasi moja tu ya kurejea katika timu ya taifa ya Ujerumani kabla ya kustahafu soka lake la kimataifa.

Loew alisema atamuita Ballack kwa mara ya mwisho kikosini kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Brazil utakaochezwa August 10 huku lengo kubwa likiwa ni kuwaaga mashabiki wake na kutoa heshima zake za mwisho akiwa kama nahodha.

Kauli hiyo ilipingwa vikali na Ballack ambapo alihoji kwamba mchezo huo wa kirafiki ulifahamika siku nyingi sasa iweje hii leo kocha huyo autumie kama sehemu ya kutaka kumlazimisha kustahafu soka la kimataifa?

Ballack kwa sasa ana umri wa miaka 34, na amekua na wakati mgumu wa kurejea katika timu ya taifa ya Ujerumani kufuatia majeraha ya mara kwa mara yanayomkabili sambamba na kupata upinzani mkali kutoka kwa viungo wa klabu ya Real Madrid Mesut Ozil pamoja na Sami Khedira.

No comments:

Post a Comment