Tuesday, March 29, 2011

UINGEREZA 1 GHANA 1: ASAMOAH GYAN AIBEBA GHANA DAKIKA ZA MWISHO.

Wachezaji wa timu ya Taifa ya Ghana wakishangilia mara baada ya mshambuliaji wa timu hiyo Asamoah Gyan kuisawazishia timu yake bao dhidi ya Uingereza na kupelekea timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa katika Uwanja wa Wembley, London, Uingereza usiku huu.

Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Uingereza Andy Carroll akishangilia mara baada ya kuifungia timu yake bao la kuongoza dhidi wakati timu hizo zilipocheza usiku huu. 

Carroll akiachia shuti kali la mguu wa kushoto lililompita kipa wa Ghana Richard Kingston na kutinga wavuni.

Mashabiki wa Ghana wapatao 18,000 waliohudhuria mchezo huo kuishangilia timu yao usiku huu.

Golikipa wa Uingereza Joe Hart akiokoa hatari langoni mwake katika mchezo huo.

Winga wa Uingereza Ashley Young akipiga shuti kali huku beki wa Ghana akijaribu kumzuia, shuti hilo la  mchezaji liliokolewa na golikipa Kingston.

Mchezaji wa Ghana Derek Boateng na mchezaji wa Uingereza Joleon Lescott wakichimbana mikwara katika mchezo baina ya timu hizo jana usiku.


Matokeo ya michezo mingine ya kimataifa ya kirafiki:

Belarus 0-1 Canada

China PR 3-0 Honduras

Colombia 0-2 Chile

Cyprus 0-1 Bulgaria

Ecuador 0-0 Peru

England 1-1 Ghana

France 0-0 Croatia

Germany 1-2 Australia

Greece 0-0 Poland

Portugal 2-0 Finland

Qatar 1-1 Russia

Rep of Ireland 2-3 Uruguay

Slovakia 1-2 Denmark

Ukraine 0-2 Italy


TP MAZEMBE KUTUA IJUMAA.

DAR ES SALAAM, Tanzania
KIKOSI kamili cha timu ya TP Mazembe kutoka DRC kinatarajiwa kutua nchini Ijumaa April 1 mwaka huu kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano ya michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika dhidi ya timu ya Simba katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Clinford Ndimbo alisema maandalizi kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Jumapili Aprili 3 yapo katika hatua za mwisho.

Alisema uongozi wa timu Mazembe umesema kuwa timu itawasili Ijumaa lakini hawakutaja muda wala mahali watapofikia ingawa tayari Simba wameshawaandalia mahala pa kufukia kama wenyeji wao.

Alisema viingilio katika mchezo huo vitakuwa kama ifuatavyo ambapo VIP "A" kiingilio kitakuwa shs. 40,000, VIP "B" shs. 20,000, VIP "C" shs. 10,000, Blue Mzunguko shs. 7,000 na Kijani mzunguko shs. 5,000.

KUNDI LA TAIFA STARS LAZIDI KUWA GUMU.

ALGERS, Algeria
MSIMAMO wa kundi D la michuano ya fainali za mataifa ya bara la Afrika iliyo katika hatua ya kufuzu umeendelea kuziweka timu za kundi hilo kwenye wakati mgumu baada ya timu ya taifa ya Algeria kupata ushindi dhidi ya timu ya taifa ya Morocco hapo jana.

Algeria wakicheza nyumbani walifanikiwa kupata ushindi wa bao moja kwa sifuri lililofungwa kwa njia ya mkwaju wa penati na Hassan Yebda katika dakika ya tano ya mchezo hali ambayo inaifanya timu hiyo kufikisha point nne sawa na timu nyingine.

Kufuatia hatua hiyo timu ya taifa ya Jamhuri ya Afrika ya kati inaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ambapo mpaka sasa imeshakufungwa mabao mawili na kufunga mabao matatu, huku Tanzania ikishika nafasi ya pili kwa kuwa na point nne huku ikiwa imefunga mabao matatu na kufungwa matatu.

Timu ya taifa ya Morocco inakamata nafasi ya tatu kwa kufikisha point nne, imefunga bao moja na kufungwa bao moja na timu ya taifa ya Algeria inakamata nafasi ya nne kwa kuwa na point nne, mabao mawili ya kufunga na mabao matatu ya kufungwa.

Michezo inayofuata ya kundi hilo itachezwa kati ya June 3-5 ambapo Tanzania watafanya ziara huko Barthelemy Boganda Stadium, mjini Bangui kwa kucheza na Jamuhuri ya Afrika ya kati na Algeria watasafiri hadi mjini Rabat kwenye uwanja wa Moulay Abdellah kucheza na timu ya taifa ya Morocco.

Wakati huo huo michezo ya kuwania kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2012 iliendelea jana ambapo:

Msumbiji 0 - 2 Zambia
Congo Brazzaville 0 - 3 Ghana
DR Congo 3 - 0 Mauritius
Madagascar 1 - 1 Guinea
Niger 3 - 1 Sierra Leone
Sudan 3 - 0 Swaziland
Ivory Coast 2 - 1 Benin
Nigeria 4 - 0 Ethiopia

ESSIEN KUONGOZA SAFU YA WASHANGILIAJI WEMBLEY LEO.

LONDON, England
KIUNGO wa klabu ya Chelsea ya nchini Uingereza Michael Essien amesema atakua miongoni mwa mashabiki watakaohudhuria kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya timu ya taifa ya Ghana dhidi ya timu ya taifa ya Uingereza utakaochezwa leo katika Uwanja wa Wembley, London.

Essien ametangaza dhamira hiyo huku akitanabaisha wazi kwamba yeye ni shabiki wa timu ya taifa lake hivyo hatosita kuelekea uwanjani kuungana na mashabiki wengine wa timu ya taifa ya Ghana ambayo ilishindwa kuandika historia ya kutinga kwenye hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2010 baada ya kutolewa na timu ya taifa ya Uruguay katika hatua ya robo fainali.

Alisema hana budi kufanya hivyo na katu hana ubaya na yoyote ndani ya timu ya taifa ya Ghana pamoja na viongozi wa GFA kufuatia maamuzi aliyoyachukua ya kukaa pembeni kwa muda kabla ya kurejea kikosini kujiunga na wengine ndani ya Black Stars.

Hata hivyo Essien ametoa sababu za kuchukua maamuzi ya kujiweka pembeni ambapo alisema kipindi hiki anakitumia kama sehemu ya kuupumzisha mwili wake baada ya kuumia magoti yote mawili akiwa na timu ya taifa ya Ghana ambayo aliiwezesha kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2010.

Ghana wanaingia uwanjani hiyo kesho huku wakiwa na kumbu kumbu nzuri ya kushinda mchezo wao wa kufuzu kucheza fainali za mataifa ya bara la Afrika za mwaka 2012 kwa kuifunga timu ya taifa ya Congo Brazzaville mabao matatu kwa sifuri.

BARRY KUKIONGOZA KIKOSI CHA ENGLAND DHIDI YA GHANA LEO.

LONDON, England
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa Uingereza Fabio Capello amemteua kiungo wa klabu ya Manchester City Gareth Barry kuwa nahodha wa kikosi chake ambacho leo kitarejea uwanjani kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Ghana.

Capello amefanya mabadiliko hayo ya baada ya kumuondoa kikosini John Terry pamoja na Frank Lampard kufuatia sababu za kuwa majeruhi baada ya kucheza mchezo wa kimataifa wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya timu ya taifa ya Wales.

Sababu nyingine ilipelekea kocha huyo wa kimataifa toka nchini Italia kumteua Barry kuwa nahodha ni kutokana na kurejea mapema kwa Wayne Rooney, kwenye klabu yake ya Manchester united ambayo inajukumu zito la kuhakikisha inashinda michezo yote ya ligi iliyosalia kwa ajili ya kujihakikishia nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

Barry mwenye umri wa miaka 30, atapata nafasi ya kuwa kiongozi wa kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza ambacho kesho atakitumikia kwa mara ya 46 na kumbu kumbu zaonyesha kwamba mchezaji huyo alishawahi kuwa nahodha mwezi uliopita pindi The Three Lion walipocheza na timu ya taifa ya Denmark.

Barry amesema kuteuliwa kwake kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza amekuchukulia kama sehemu ya kuboresha historia ya sola lake lakini bado akaanisha wazi kwamba kila mmoja ndani ya kikosi chao ni kiongozi.

Katika hatua nyingine Capello amesema kesho kikosi chake kitakua na mabadiliko makubwa huku akitarajia kumuanzisha mshambuliaji wa klabu ya Liverpool Andy Carroll.

Katika safu ya ulinzi atakuwepo Gary Cahill, Phil Jagielka pamoja na Leighton Baines, huku kipa Joe Hart pamoja na Scott Parker wakitegemea kuendelea kuwepo kikosini kama kawaida.

"CARROLL, SUAREZ WAMEIMARISHA KIKOSI KULIKO ALIPOKUWA TORRES." GERRARD.

LONDON, England
NAHODHA na kiungo wa klabu ya Liverpool Steven Gerrard amesema usajili uliofanywa na meneja wa klabu hiyo Kenny Dalglish katika msimu wa dirisha dogo umeziba nafasi ya mshambuliaji alieondoka klabuni hapo na kujiunga na klabu ya Chelsea Fernando Torres.

Gerrard amesema ujio wa Andy Carroll pamoja na Luis Suárez umebadilisha mtazamo wa kikosi cha Liverpool ambacho mwanzoni mwa msimu huu kilidhaurika na kila mmoja kufuatia matokeo mambovu yaliyokua yakiwaandama.

Alisema bado Torres ni mchezaji mzuri na anaekidhi viwango vya kuongoza safu ya ushambuliaji lakini ukweli ni kwamba bado wana haki ya kujivunia usajili wa wachezaji hao wawili uliofanywa mwezi januari.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30 pia amesisitizia suala la meneja wao kwa sasa Dalglish ambapo amesema anastahili kuendelea kusali kikosini kutokana na kazi nzuri aliyoifanya tangu alipokichukua kikosi kutoka mikononi mwa Roy Hodgson mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema Dalglish anapendwa na kila mmoja klabuni hapo na katu hatojisikia vyema endapo meneja huyo wa kimataifa toka nchini Scotland ataondoka mwishoni mwa msimu huu kama mkataba wake unavyoeleza.

Gerrard ameeleza wazi kwamba wakati Rafael Benitez akitimuliwa kazi mwishoni mwa msimu uliopita klabuni hapo nao walikua katika wakati mgumu wa kufikiria nani atakuwa mbadala wa meneja huyo toka nchini Hispania ambapo majina mengi yalisikika toka kwenye vyombo mbali mbali vya habari.

Monday, March 28, 2011

SCOTLAND YASHINDWA KUTAMBA KWA BRAZIL.

Mshambuliaji kinda wa Brazil Neymar akipiga mpira ambao beki huyo wa Scotland aliunawa na kusababusha Penati wakati timu hizo zilimenyana katika Uwanja wa Emirates, Uingereza jana usiku. Brazil ilishinda 2-0.

Golikipa wa Scotland akiufuata mpira bila matumaini na kutinga wavuni kuandika bao la kwanza la Brazil.

Neymar akipiga penati kuindikia timu yake ya Brazil bao la pili dhidi ya Scotland.

Mchezaji Nguli wa Brazil ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika mchezo ulizikutanisha timu hizo akipunga mkono kwa mashabiki.

Mashabiki wakijiandaa kuingia Uwanjani kushuhudia mchezo kati ya Brazil na Scotland.

"FABREGAS HANA NAFASI BARCELONA." TORRES

LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa Chelsea Fernando Torres ameweka wazi kuwa kiungo wa Arsenal Cesc Fabregas atakuwa ni chaguo zuri kwa Barcelona kama wakiamua kumsajili ingawa hadhani kuwa timu hiyo inahitaji kusajili kiungo kwa sasa.

"Sijui kama Barcelona wanamhitaji mchezaji kama Fabregas. Hiyo ni juu ya Kocha pep Guardiola kuamua. Sifuatilii kwa karibu Ligi ya Hispania. Ni vigumu kuiweka sawa timu kama Barcelona na nani atatoka kama wakimsajili Fabregas," alisema torres akihojiwa na gazeti moja la Hispania.

"Ni mchezaji wa kweli wa timu hiyo hatahivyo na chaguo zuri kama akisajiliwa. Cesc anaheshimika zaidi Uingereza kuliko Hispania, kwasababu hajawahi kucheza Hispania. watu hapa Uingereza wamhesabu kama mmoja wa wachezaji watatu bora Uingereza.

"ILIBAKI KIDUCHU NICHUKUE MIKOBA YA KUINOA ENGLAND." MOURINHO

MADRID, Hispania
KOCHA wa Real Madrid Jose Mourinho amethibisha kuwa yalikuwa yamebaki masaa machache kukubali kukinoa kikosi cha timu ya Taifa ya Uingereza kabla moyo wake haujasita kufanya hivyo katika dakika za mwisho.

Kocha huyo anayejulikana kwa jina la "The Special One" ailikiri kuwa alikuwa tayari kukubali ofa ya kuifundisha England, baada ya kuondoka Chelsea.

Kocha huyo raia wa Ureno ambaye aliondoka Chelsea Septemba 2007, miezi miwili kabla kocha wa Uingereza kwa kipindi hicho Steve McClaren hajatimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Fabio Capello, alifafanua kuwa aliamua dakika za mwisho kuwa bado anapendelea kuwa kocha wa vilabu.

Akihojiwa na gazeti moja la Ufaransa alisema kuwa ilikuwa imebaki saa moja kabla sijaingia mkataba na Uingereza.

Aliendelea kusema kuwa katika dakika za mwisho alianza kuifikiria kazi yake mpya hiyo ya kufundisha timu ya taifa, ambapo atakuwa na mechi moja katika mwezi muda wote atakuwa akiutumia ofisini au kufuatilia mechi zingine halafu atasubiria mpaka yatakuja mashindano kama ya Ulaya au Kombe la Dunia nikaona hii kazi hainifai.

FIFA KUTUMIA TEKNOLIGIA YA VIDEO KOMBE LA DUNIA 2014.

ZURICH, Switzerland
RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Sepp Blatter amethibitisha kuwa teknologia ya video itaweza kutumika katika fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil, akiongezea kuwa taratibu kwajili ya mfumo utakuwa umekamilika katika kipindi cha mashindano hayo.

Kwa kawaida katika mchezo wa soka huwa hakutakiwi kuwa na matumizi ya teknologia, Lakini Blatter alikiri kuwa kuna mabaliko inabidi yafanyike.

Uingereza ndio walikuwa wahanga katika Kombe la Dunia lililofanyika mwaka uliopita Afrika ya Kusini walipokataliwa bao ambalo lilionekana kabisa kuingia nyavuni tukio ambalo kama teknologia ya video ingetumika basi lingekuwa bao.

Akihojiwa Blatter alisema kwamba anafikiri ifikapo mwaka 2012 mfumo huo utakuwa tayari kutambua kama bao litakuwa limefungwa au la kabla ya kuanza kutumia katika fainali za Kombe la Dunia 2014, Brazil.

"Ni muhimu kufungua mjadala mpya kuhusu hili ili kuepusha Waingereza kuendelea kukosa haki yao." alimalizia kwa utani Blatter.

ADEBAYOR AKANUSHA KUREJEA TOGO.

MADRID, Hispania
MSHAMBULIAJI wa klabu ya Manchester city ambae kwa sasa anaitumikia klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania kwa mkopo Emmanuel Adebayor amekanusha taarifa za yeye kuwa mbioni kurejea kwenye timu ya taifa ya Togo ambayo mwishoni mwa juma hili itaendelea na kampeni ya kusaka nafasi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2012 kwa kucheza na timu ya taifa ya Malawi.

Adebayor amekanusha taarifa hizo baada ya Raisi wa Shirikisho la Soka nchini Togo Gabriel Ameyi kueleza wazi kwamba mshambuliaji huyo atajiunga na kikosi cha timu ya taifa kufuatia kumaliza dhamira yake ya kustahafu soka la kimataifa.

Adebayor alisema hakuwahi kubadili msimamo wake wa kutokuichezea timu ya taifa ya Togo na ameshangazwa na kitendo cha Kocha Mkuu Stephen Keshi kumjumuisha kwenye kikosi chake kitakachoshuka uwanjani mwishoni mwa juma hili.

Ameyi alivieleza vyombo vya habari kwamba mshambuliaji huyo alibadili msimamo baada ya kukutana nae mjini Madrid na kufanya mazungumzo ya muda.

Adebayor alitangaza kustahafu soka la kimataifa baada ya timu ya taifa ya Togo kushambuliwa na waasi wa mji wa kabinda nchini Angola mwanzoni mwa mwaka jana wakati timu hiyo ilipokua safarini kushiriki fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2010.

NIGERIA, ARGENTINA USO KWA USO JUNE MOSI.

ABUJA, Nigeria
TIMU ya taifa ya Nigeria itacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa zamani wa dunia timu ya taifa ya Argentina June mosi mwaka huu.

Rais wa Shirikisho la Soka nchini humo Aminu Maigari alisema taratibu za kuchezwa kwa mchezo huo tayari zimeshakamilika na wana imani Argentina itawaongezea kasi katika harakati za kusaka nafasi ya kushiriki fainali za mataifa ya bara la Afrika kwa mwaka 2012 ambapo Super Eagles watarejea tena uwanjani June 4/5 kucheza na timu ya taifa ya Ethiopia.

Alisema mchezo huo utachezwa mjini Abuja katika Uwanja wa taifa na watauchukulia kama sehemu ya kutaka kulipiza kisasi cha kufungwa bao moja kwa sifuri kwenye fainali za kombe la dunia ambapo Nigeria walipangwa katika kundi moja na Argentina.

SAHA AHOFIA KUSHINDWA KUMALIZIA MSIMU HUU.

LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa kimataifa toka nchini Ufaransa na klabu ya Everton Louis Saha amesema hadhani kama atarejea tena uwanjani msimu huu kufuatia maumivu ya kifundo cha mguu aliyoyapata mwishoni mwa juma lililopita.

Saha ametoa mtazamo huo huku klabu yake ikionyesha nia ya kutaka kumuona anarejea tena uwanjani kuisaidia katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu.

Alisema alijisikia maumivu makali sana baada ya kuumia kifundo cha mguu akiwa kwenye mchezo wa ligi mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Fulham na mpaka sasa hali yake bado haitabiriki hivyo hadhani kama anaweza kuuwahi muda wa ligi uliosalia.

Hatua hiyo pia inaonekana kumpa wakati mgumu meneja wa klabu ya Everton David Moyes hasa ikizingatiwa kikosi chake kwa sasa kinaendelea kuwakosa wachezaji muhimu kama Saha pamoja na wachezaji wengine waliopo kwenye benchi la majeruhi.

Alipojiwa juu ya matarajio yake kwa mchezaji huyo Moyes alishindwa kuthibitisha lolote zaidi ya kusema anasubiri taarifa za majibu kutoka kwa daktari ambazo zitaainisha Saha atakuwa nje kwa muda gani.

Kikosi cha klabu ya Everton kwa sasa kinashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza na endapo kitaendelea kupanda zaidi ya hapo huenda kikapata nafasi ya kucheza michuano ya barani ulaya msimu ujao.

Friday, March 25, 2011

BAFANA BAFANA MBIONI KUBADILISHWA.

Mshambuliaji wa Bafana Bafana Bongani Khumalo akishangilia mara baada ya kufunga bao dhidi ya timu ya Ufaransa katika Kombe la Dunia.

PRETORIA, South Africa
TIMU ya Taifa ya Afrika Kusini ipo mbioni kuliacha kulitumia jina la utani la Bafana Bafana kwa sababu halihamasishi vya kutosha.

Waziri wa Michezo wa nchi hiyo, Fikile Mbalula badala ya kutumia jina la Bafana Bafana hivi sasa wanaangalia uwezekano wa kutumia kati ya majina matano ya wanyama maarufu nchini humo ambayo ni Kiboko (Buffalo), Simba (Lion), Kifaru (Rhino), Chui (Leopard) na Tembo (Elephant).

STARS NDANI YA KIBARUA KIZITO NA AFRIKA YA KATI.

Nahodha wa Stars Shadrack Nsajigwa (kushoto), Kocha Mkuu wa Stars Jen Poulsen (katikati) na Kocha wa timu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati Accorsi Jules, wakiongea na waandishi wa habari kuhusu mchezo wao wa kesho. 

DAR ES SALAAM, Tanzania
TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kesho itakuwa na kibarua kizito cha kuivaa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hii itakuwa ni nafasi pekee kwa Stars kujaribu nafasi yao haswa ikizingatiwa watakuwa wakicheza mbele ya maelfu ya mashabiki hapa nyumbani ili kujiweka katika nafasi ya kushiriki michuano hiyo.

Timu ya Afrika ya Kati nayo haitakubali kirahisi haswa ikizingatiwa rekodi yao nzuri ya michezo iliyopita ambapo walitoa suluhu na Morocco ugenini kabla ya kuisindilia mabao 2-0 Algeria nyumbani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kocha Mkuu wa Stars Jen Poulsen alisema kikosi chake kimejiandaa vyema na kiko tayari kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu lakini unaweza kuwa na matokeo mazuri.

Poulsen alisema karibu wiki mbili kikosi chake kimekuwa katika maandalizi kabambe ambapo alisema hakuna tatizo la majeruhi linalomsumbua kwa sasa na wachezaji wamejiandaa vyema kimazoezi na kiakili kwa ajili ya mchezo huo muhimu.

Naye Nahodha wa Stars Shadrack Nsajigwa alisema kwa niaba ya wenzake kwamba wamejiandaa vyema na wako tayari kwa ajili ya mchezo na kuahidi ushindi katika mchezo huo, japo aliwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi ili kuishangilia timu yao.

Mbali na Stars na Afrika ya Kati michezo mingine itakayochezwa kesho ya kutafuta tiketi ya michuano hiyo katika nchi mbalimbali barani Afrika ni kama ifuatavyo:

Chad vs Botswana
Mali vs Zimbabwe
Madagascar vs Guinea
Burkina Faso vs Namibia
Rwanda vs Burundi
Cape Verde vs Liberia
Guinea Bissau vs Uganda
Sudan vs Swaziland
Libya vs Comoros
Niger vs Sierra Leone

ABIDAL ARUHUSIWA KUTOKA HOSPITALINI BAADA YA UPASUAJI.

BARCELONA, Hispania
BEKI wa Barcelona Eric Abidal ameruhusiwa kutoka hospitali na kurudi nyumbani ambako anaendelea kujiuguza baada ya kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe katika ini lake wiki iliyopita.

Abidal (31) anatarajiwaa kuanza mazoezi baada ya wiki nne ili aweze kurudi tena uwanjani.

Taarifa kutoka mtandao wa klabu hiyo ilisema mchezaji huyo aliruhusiwa kutoka hospitalini jana usiku na yupo nyumbani kwake kwa mapumziko ambapo iliendelea kusema kuwa kulikuwa hakuna tatizo lolote lilijitokeza katika upasuaji huo.

Msimu huu Abidal ameichezea timu yake mechi 22, zikiwemo na mechi saba za Ligi ya Mabingwa Ulaya na mkataba wake na Barca unakwisha 2012.

Thursday, March 24, 2011

ALVES AONGEZEWA MKATABA BARCA.

BARCELONA, Hispania
BEKI wa pembeni wa kimataifa toka nchini Brazil Daniel Alves amekubalia kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuwatumikia mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona.

Alves amekubali kusaini mkataba huyo baada ya kueleza wazi mipango yake mara baada ya msimu huu kumalizika ambapo maamuzi aliyotaka kuyachukua ni kuihama klabu hiyo ya nchini Hispania na kusaka klabu nyingine huku tegemeo lake kubwa likiwa Man City.

Mkataba utakaosainiwa na beki huyo mwenye umri wa miaka 27 utamuwezesha kuendelea kuitumikia Barcelona hadi mwezi June mwaka 2015.

Mbali na kueleza mipango yake ya kutaka kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu pia mchezaji huyo alionyesha kuchukizwa na hatua ya viongozi wa Barca ambao hawakumuonyesha ushirikiano wa kutosha wa kumthibitishia kama wapo tayari kukaa nae mezani na kumaliza mara moja suala hilo.

Alves alisajiliwa na Fc Barcelona mwishoni mwa msimu wa mwaka 2007-08 akitokea Sevilla na tayari ameshaitumikia klabu hiyo ya Catalunya katika michezo 141.

BALLACK AOMBA RADHI.

LEVERKUSEN, ujerumani
KIUNGO wa klabu ya Bayer Leverkusen Michael Ballack amelazimika kuomba radhi kupitia mtandao wa klabu hiyo kufuatia kulishawishi kundi la mashabiki wa Factory Squad kutoa maneno makali kwa mashabiki wa mjini Cologne waliokua wamehudhuria kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Schalke 04 mwishoni mwa juma lililopita.

Ballack alitoa maneno makali kwa mashabiki hao baada ya kikosi cha Bayer Leverkusen kupata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri kwenye uwanja wa BayArena ambapo alidiriki kufanya hivyo kwa kutumia kipaza sauti.

Alisema anajutia kosa alilolifanya na hana budi kusamehewa kutokana na mazingira yaliyokuwepo uwanjani hapo baada ya kikosi chao kufanikiwa kuzipata point tatu muhimu.

Kitendo hicho kilichofanywa na Ballack huenda kikaishawishi kamati ya nidhamu ya chama cha soka nchini Ujerumani kumuadhibu kiungo huyo ambae bado msaada wake unahitajika katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa ligi.

MOURINHO BADO AVUTIWA NA LIGI KUU UINGEREZA.

MADRID, Hispania
KOCHA wa kimataifa toka nchini Ureno pamoja na klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania José Mourinho, ameendelea kusisitizia jambo la kurejea tena nchini Uingereza kuitumikia moja ya klabu kubwa inayoshiriki ligi kuu.

Mourinho ameendelea kutoa msisizo huo alipohojiwa na shirika la utangazaji la nchini Uingereza BBC ambapo alisema dhamira hiyo inatokana na kuyapenda sana maisha ya nchini humo ambapo aliishi kwa muda wa miaka minne akiwa na kikosi cha klabu ya Chelsea.

Alisema kwa sasa ni vigumu kueleza wazi ni lini anatarajia kurejea nchini Uingereza kutokana na mkataba wa miaka minne alioingia na uongozi wa klabu ya Real Madrid mwishoni mwa msimu uliopita lakini ukweli ni kwamba baada ya kuondoka nchini Hispania hatokwenda popote zaidi ya kurejea kwenye himaya ya malkia Elizabeth.

Mourinho pia amzungumzia hatua ya kikosi chake kupangwa na klabu ya Tottenham Hotspurs kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya ambapo alisema hakujihisi vibaya bali alilipokea suala hilo kwa mikono miwili.

Alisema aliomba usiku na mchana kutosikia wala kuona anapangwa na klabu ya Chelsea ama Inter Milan na endapo ingetokea hivyo angekua na mazingira magumu sana kutokana na mapenzi yeke dhidi ya klabu hizo mbili ambazo amezipa mafanikio makubwa.

Hata hivyo Mourinho ameeleza kwamba Tottenham Hotspurs ni klabu yenye ushindani na imeleta changamoto mpya kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya kufanikiwa kuzifunga klabu za mjini Milan ambazo ni Inter Milan pamoja na AC Milan.

Katika hatua nyingine meneja huyo alisema ana uhakika kiungo wa kikosi chake toka nchini Ureno Cristiano Ronaldo ambae mwishoni mwa juma lililopita alijitonesha maumivu ya nyama za paja atauwahi mchezo huo wa hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya utakaochezwa mwanzoni mwa mwezi ujao.

BENDTNER AUMIA MAZOEZINI.

AMSTERDAM, Uholanzi
MSHAMBULIAJI wa kimataifa toka nchini Denmark na klabu ya Arsenal Nicklas Bendtner hii leo amelazimika kurejeshwa kambini baada ya kuumia akiwa katika maandalizi na wachezaji wenzake wa timu ya taifa kabla ya mpambano wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya timu ya taifa ya Norway.

Bendtner amefikia hatua hiyo kufuatia kuumia kifundo cha mguu wake wa kulia na taarifa zaidi juu ya jeraha linalomkabili zitatolewa baadae baada ya majibu ya vipimo vya picha za x-Ray kueleza wazi.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 amefikwa na maswahibu hayo alipokua kwenye heka heka za kukimbia mbio za kawaida kabla ya kujiunga wachezji wengine tayari kwa mazoezi kamili toka kwa kocha mkuu wa timu ya taifa ywa Denmark Morten Olsen.

Kuumia kwa, Bendtner kunaendelea kuzua hofu kwa klabu yake ya Arsenal ambayo ipo kwenye nafasi nzuri ya kuwanai taji la ligi kuu ya soka nchini Uingereza msimu huu kufautia utofauti wa point nne uliopo kati ya The Gunners dhidi ya Man Utd.

VAN BOMMEL NJE KIKOSI CHA UHOLANZI.

AMSTERDAM, Uholanzi
NAHODHA na kiungo wa timu ya taifa ya Uholanzi Mark van Bommel hatojumuishwa kwenye kikosi kitakacho endelea na kampeni ya kusaka nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya za mwaka 2012 kwa kucheza na timu ya taifa ua Hungary mwishoni mwa juma hili kutokana na sababu za kuwa majeruhi.

Van Bommel ataukosa mchezo huo wa kundi la tano kufuatia jeraha la paja linalomsumbua kwa sasa lakini bado imeelezwa ataendelea kusalia kambini kwa ajili ya mchezo wa March 29 ambapo Uholanzi watakua nyumbani wakirejeana na timu ya taifa ya Hungary.

Wachezaji wengine wa timu ya taifa ya Uholanzi ambao tayari wameshatemwa kikosini kufautai sababu za kuwa majeruhi ni pamoja na Arjen Robben, Klaas Jan Huntelaar pamoja na Hedwiges Maduro.

Wednesday, March 23, 2011

MUNTARI HATIHATI KUIVAA UINGEREZA.

LONDON, England
KIUNGO wa klabu bingwa barani Ulaya Inter Milan ambae anaitumikia klabu ya Sunderland ya nchini Uingereza kwa mkopo Suleyman Muntari amezusha hofu kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ghana kinachojiandaa na mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya bara la Afrika kwa kucheza na timu ya taifa ya Congo Brazzaville pamoja na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Uingereza.

Kiungo huyo amezusha hofu hiyo baada ya kuumia kiazi cha mguu mwishoni mwa juma hili alipokua kwenye mchezo wa ligi ambapo Sunderland walikubali kisago cha mabao 2-0 toka kwa Liverpool huko Stadium of Lights.

Tayari meneja wa klabu ya Sunderland Steve Bruce ameshaeleza kwamba hadhani kama kiungo huyo atakua na nafasi ya kutosha ya kucheza michezo ya kimataifa kwa katika kipindi hiki cha juma moja na nusu.

Katika hatua nyingine kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ghana Goran Stevanovic, amejiandaa kuikabili timu ya taifa ya Uingereza pasipokua na kiungo wa klabu ya Chelsea Michael Essien ambae ameweka msimamo wa kutokua tayari kurejea katika kikosi cha timu ya taifa kwa sasa.

Hata hivyo kocha huyo bado anaamini Essien atabadili msimamo huo na kurejea kwenye kikosi cha timu ya taifa lake ambacho hajawahi kukitumikia kwa muda wa mwaka mmoja sasa.

LAZIO YAWEKA MATUMAINI YA KUCHEZA ULAYA MSIMU UJAO.

LAZIO, Italia
UONGOZI wa klabu ya Lazio ya nchini Italia unaaminikikosi chao kina uwezo mkubwa ya kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao bila ya kuwa na kiungo wa kimataifa toka nchini Brazil Matuzalém Francelino da Silva.

Imani hiyo kwa viongozi wa Lazio imekuja baada ya Silva kuongezewa adhabu na kamati ya nidhamu ya Chama cha Soka nchini Italia kufuatia kosa alilolifanya katika mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Cecena waliokubali kisago cha bao 1-0 kilichotolewa huko Stadio Olympico.

Kamati ya nidhamu ya chama cha soka nchini Italia imetoa taarifa za kumuongezea adhabu kiungo huyo kutoka mchezo mmoja hadi mitatu baada ya kufuatilia picha za televisheni za mchezo huo na kubainika kwamba Silva alimsukuma kwa makusudi kiungo wa klabu ya Cecena Antonio Jimenez pindi timu hizo zipokutana mwishoni mwa juma lililopita.

Kwa sasa Lazio wanakamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ya nchini Italia kwa kufikisha point 54 huku michezo minane ikisalia.

Kamati ya nidhamu ya chama cha soka nchini Italia pia imethibitisha kwamba beki wa kimataifa toka nchini Brazil na klabu ya Inter Milan Lucio hatocheza mchezo ligi utakaomua nani ataelekea kileleni kati ya mahasimu wawili wa jiji la Milan AC Milan dhidi ya mabingwa watetezi.

Lucio ataukosa mchezo huo wa April mbili kufuatia kadi ya njano aliyoonyeshwa mwishoni mwa juma lililopita kwenye mchezo dhidi ya Lecce hali ambayo inamfanya kuwa na kadi tano za njano.

UCHAGUZI FIFA: BLATTER KUACHIA NGAZI 2015, BIN HAMMAN AKALIA KOONI.

NYON, Switzerland
RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Sepp Blatter amepanga kuachia ngazi mwaka 2015 endapo atachaguliwa kuliongoza shirikisho hilo katika uchaguzi wa mwezi June mwaka huu.

Blatter mwenye umri wa miaka 75 ametoa msimamo huo alipopata nafasi ya kuhutubia kwenye mkutano wa Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) unaofanyika mjini Nyon nchini Uswis.

Alisema endapo atapa kipindi kingine cha miaka minne cha kuiongoza FIFA atakua na umri mkubwa zaidi hivyo hatokua na budi kuachia nafasi kwa wengine waendeleze pale atakapoachia.

Mohamed Bin Hamman.
Hata hivyo kiongozi huyo ambae aliingia madarakani mwaka 1998, tayari anakabiliwa na upinzani wa hali ya juu kutoka kwa raisi wa Shirikisho la Soka barani Asia Mohamed Bin Hammam alitangaza dhamira hiyo mwishoni mwa juma lililopita.

Suala kubwa linalopigiwa upatu na Mohamed Bin Hammam ambalo linachukuliwa kama sehemu inayomtia hofu kwa Blater ni usiri mkubwa uliokithiri ndani ya FIFA ambao unatakiwa kukomeshwa na uongozi wa mdau huyo wa soka kutoka nchini Qatar endapo atachaguliwa.


Akihojiwa Hammam alisema wadau wa soka ulimwenguni kote wanastahili kufahamu suala lolote linaloendelea ndani ya FIFA pasipo kufichwa na hivyo utawala wake utahakikisha unalitimiza hilo na kuondoa dhana ya kuongoza mpira kama ilivyo katika Nyanja za siasa.

Alisema jibu kubwa ya kumaliza mzozo huo ni kuundwa kwa kamati ya kuweka masuala mbali mbali hadharani ambayo itakua ikifanya kazi yake bila kwa kwenda sambamba na tukio husika aidha liwe la faida ama hasara ndani ya FIFA.


Tuesday, March 22, 2011

JARVIS AITWA KWA YA KWANZA UINGEREZA KUZIBA PENGO LA WALCOTT NA JOHNSON.

LONDON, England
WINGA wa klabu ya Wolves Hampton Wanderers Matt Jarvis amefanikiwa kuitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza ambacho juma hili kitaingia kambini kujiandaa na mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya bara la Ulaya dhidi ya timu ya taifa ya Wales na kisha mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi yua timu ya taifa ya Ghana.

Winga huyo mwenye umri wa miaka 24 ameitwa kikosini na kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza was Fabio Capello kufuatia kuumia kwa winga wa klabu ya Arsenal Theo Walcott pamoja na Adam Johnson wa klabu ya Man City.

Hata hivyo kuitwa kwa Matt Jarvis bado kunatoa changamoto kwa mawinga wengine waliojumuishwa kwenye kikosi hicho chenye wachezaji 26, Aaron Lennon pamoja na Ashley Young ambao huenda wakaanzishwa katika kikosi cha kwanza.

Mtandaji mkuu wa klabu ay Wolves Hampton Wanderers Jez Moxey amesema wamefurahishwa na kitendo cha mchezaji huyo kuitywa kwenye kikosi cha timu ya taifa hatua mbayo wanaichukuliwa kama sehemu ya kukua kwa klabu yao licha ya kuendelea kuburuza mkia kwenye msimamo wa ligi.

Nae mshambuliaji mpya wa klabu ya Liverpool Andy Carroll, ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza baada ya kupona jeraha la paja ambapo kwa mara ya kwanza aliichezea timu hiyo kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Ufaransa mwezi Novemba mwaka jana.

Kikosi kamili cha Uingereza upande wa:

Makipa: Joe Hart (Manchester City), Ben Foster (Birmingham City), Robert Green (West Ham United)

Mabeki: Glen Johnson (Liverpool), John Terry (Chelsea), Phil Jagielka (Everton), Ashley Cole (Chelsea), Kyle Walker (Tottenham Hotspur - on loan at Aston Villa), Gary Cahill (Bolton Wanderers), Michael Dawson (Tottenham Hotspur), Joleon Lescott (Manchester City), Leighton Baines (Everton)

Viungo: Aaron Lennon (Tottenham Hotspur), Jack Wilshere (Arsenal), Frank Lampard (Chelsea), Ashley Young (Aston Villa), James Milner (Aston Villa), Scott Parker (West Ham United), Gareth Barry (Manchester City), Stewart Downing (Aston Villa), Matthew Jarvis (Wolverhampton Wanderers)

Washambuliaji: Andy Carroll (Liverpool), Wayne Rooney (Manchester United), Darren Bent (Aston Villa), Peter Crouch (Tottenham Hotspur), Jermain Defoe (Tottenham Hotspur)

CR7 HATIHATI KUIVAA TOTTENHAM CHAMPIONS LEAGUE.

MADRID, Hispania
KIUNGO wa kimataifa toka nchini Ureno pamoja na klabu ya Real Madrid Cristiano Ronaldo atakua nje ya uwanja kwa muda wa majuma matatu yajayo kufuatia majeraha ya nyama za paja aliyoyapata katika mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita.

Kiungo huyo alilazimika kutolewa nje ya uwanja katika mchezo wa ligi dhidi ya Atletico Madrid waliokubalia kisago cha mabao mawili kwa moja na nafasi yake ilichukuliwa na muagentina Angel De Maria.

Kuumia kwa Cristiano Ronaldo kunamaanisha hatokuwepo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ureno ambacho mwishoni mwa juma hili kitacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Chile na kisha kitarejea kwenye kampeni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za ulaya za mwaka 2012 kwa kuonyeshana undava na timu ya taifa ya Finland.

Mbali na kutokuwepo katika michezo hiyo ya kimataifa Cristiano Ronaldo pia amezua hofu kubwa ya kutokuwepo katika kikosi cha Real Madrid ambacho kitacheza mchezo wa hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya dhidi ya Tottenham Hotspur April 5 mwaka huu.

Monday, March 21, 2011

LOEW AMTEMA NAHODHA WAKE KIKOSI CHA UJERUMANI.

MUNICH, Ujerumani
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo Joachim Loew amemtema kiungo na nahodha wake Michael Ballack kwenye kikosi kitakachoanza maandalizi mwanzoni mwa juma lijalo tayari kwa kuendelea na kampeni ya kusaka nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Bara la Ulaya za mwaka 2012.

Loew ametangaza kumtema kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34 baada ya kushindwa kurejea katika hali yake ya kawaida kama ilivyokua ikitarajiwa kufuatia maumivu ya mfupa wa ugoko aliyoyapata mwanzoni mwa msimu huu.

Alisema pamoja na kumtema kwenye kikosi chake ambacho kitacheza na timu ya taifa ya Kazakhstan, pamoja na Australia bado anatarajia kuketi nae chini kwa lengo la kujadili mustakabali wa maisha yake ya baadae ndani ya kikosi cha Ujerumani ambacho kilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye fainali za kombe la dunia.

Katika kikosi cha Ujerumani Loew amemrejesha kikosini kiungo wa klabu ya Bayern Munich Toni Kroos pamoja Mario Gomez ambao wote kwa pamoja waliukosa mchezo wa mwezi Februali dhidi ya timu ya taifa ya Italia kufuatia sababu za kuwa majeruhi.

Pia amemuita mshambuliaji wa klabu ya Mainz Andre Schuerrle, ambae alianza kuitumikia timu ya taifa ya Ujerumani mwaka jana huku kipa wa Werder Bremen Tim Wiese nae akichukuliwa kama kipa chaguo la tatu.

Kikosi kamili cha Ujerumani kwa upande wa;

Makipa: Manuel Neuer (Schalke 04), Rene Adler (Bayer Leverkusen), Tim Wiese (Werder Bremen);

Mabeki: Arne Friedrich (VfL Wolfsburg), Dennis Aogo (Hamburg SV), Holger Badstuber (Bayern Munich), Philipp Lahm (Bayern Munich), Jerome Boateng (Manchester City), Mats Hummels (Borussia Dortmund), Per Mertesacker (Werder Bremen), Marcel Schmelzer (Borussia Dortmund);

Viungo: Mario Goetze (Borussia Dortmund), Sven Bender (Borussia Dortmund), Mesut Ozil (Real Madrid), Sami Khedira (Real Madrid), Bastian Schweinsteiger (Bayern Munich), Christian Traesch (VfB Stuttgart), Toni Kroos (Bayern Munich), Andre Schuerrle (Mainz 05)

Washambuliaji: Mario Gomez, Miroslav Klose, Thomas Mueller (all Bayern Munich), Lukas Podolski (Cologne)

DEL BOSGUE ATAJA BUNDUKI ZAKE.

MADRID, Hispania
KOCHA Mkuu wa mabingwa wa soka duniani Hispania Vicente del Bosque, amemuita kikosini mshambuliaji wa klabu ya Valencia Juan Manuel Mata García pamoja na kiungo wa klabu ya Osasuna Javier "Javi" Martínez Aguinaga kwa ajili ta mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya za mwaka 2012.

Del Bosque amewaita kikosini wachezaji hao kwa lengo la kuziba mapengo yaliyoachwa wazi na wachezaji majeruhi ambapo kwa upande wa Juan Manuel Mata García ataziba nafasi ya mshambuliaji wa klabu ya Barcelona Pedro huku Javier "Javi" Martínez Aguinaga akitarajiwa kuziba nafasi ya kiungo wa klabu ya Arsenal Cesc Fabregas.

Beki wa klabu ya Athletic Bilbao Andoni Iraola nae amejumuishwa kikosini baada ya kukosekana kwa beki na nahodha wa klabu ya Barcelona Carles Puyol ambae bado anasumbuliwa na maumivu ya mguu wake wa kulia.

Kikosi kamili cha Hispania kilichoitwa hii leo kwa upande wa;

Makipa: Iker Casillas (Real Madrid), Victor Valdes (Barcelona), Pepe Reina (Liverpool).

Mabeki: Alvaro Arbeloa (Real Madrid), Sergio Ramos (Real Madrid), Raul Albiol (Real Madrid), Gerard Pique (Barcelona), Carlos Marchena (Villarreal), Joan Capdevila (Villarreal), Andoni Iraola (Athletic Bilbao).

Viungo: Xavi (Barcelona), Xabi Alonso (Real Madrid), Andres Iniesta (Barcelona), Javi Martinez (Athletic Bilbao), Sergio Busquets (Barcelona), Santi Cazorla (Villarreal).

Washambuliaji: David Silva (Manchester City), David Villa (Barcelona), Fernando Torres (Chelsea), Fernando Llorente (Athletic Bilbao), Jesus Navas (Sevilla), pamoja na Juan Mata (Valencia).

Kikosi cha tumu ya taifa ya Hispania mwishoni mwa juma lijalo kitaendelea na kampeni ya kusaka nafasi ya kutetea ubingwa wa barani ulaya kwa kucheza na timu ya taifa ya jamuhuri ya Czech nyumbani na kisha kitasafiri siku nne baadae kucheza na kwa ajilia ya kucheza na timu ya taifa ya Lithuania.

RUNGU LA UEFA LAHAMIA ITALIA.

MILAN, Italia
SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya (UEFA) kupitia kamati yake ya nidhamu limetangaza kumfungia michezo mitatu kiungo wa kimataifa toka nchini Italia pamoja na klabu ya AS Roma Daniele de Rossi baada ya kumbaini alifanya kosa ambalo halikutiliwa maanani na muamuzi.

Rossi amefikwa na adhabu hiyo baada ya picha za televisheni za mchezo wa marejeano wa hatua ya 16 bora ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kati ya AS Roma dhidi ya Shakter Doneski kuonyesha kuwa alimpiga kiwiko nahodha wa klabu hiyo ya nchini Ukraine Darijo Srna.

Katika taarifa iliyotolewa na kamati ya nidhamu ya UEFA imeeleza kwamba Rossi alifanya kitendo hicho kwa makusudi na hakuadhibiwa na muamuzi alichezesha mchezo huo kutokana na mazingira yaliyokuwepo uwanjani hapo.

Katika mchezo huo wa marejeano uliochezwa mjini Doneski nchini Ukraine wenyeji walipata ushindi wa mabao matatu kwa sifuri ambao uliwawezesha kutinga katika hatua ya robo fainali ambayo itawakutanisha na mabingwa wa soka nchini Hispania Fc Barcelona.

AFRIKA KUSINI YAANZA MAANDALIZI YA KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA UNDER 20, BAADA YA KUHAMISHIWA HUKO KUTOKANA NA MACHAFUKO YA LIBYA.

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
RAIS wa Chama cha Soka nchini Afrika Kusini (SAFA) Kirsten Nematandani amesema hawana budi kuzipokea kwa mikono miwili fainali za Mataifa ya Bara la Afrika zilizohamishiwa nchini humo zikitolewa nchini Libya.

Kirsten Nematandani alisema fainali hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuchangia maendeleo ya soka nchini humo na anaamini mshawasha wa mashabiki wa soka utarejea tena kama ilivyokua kwenye fainali za kombe la dunia pamoja na fainali za wanawake za barani Afrika.

Alisema baada ya kupatiwa nafasi hiyo kinachoendelea kwa sasa ni maandalizi ya viwanja ambavyo vinatakiwa kuwa tayari kabla ya kuanza kwa fainali hizo April 17 na kumalizika May 2.

Hata hivyo amekiri ubora na ubunifu wa hali ya juu ndio vimekua chanzo kwa nchi ya Afrika kusini kushinda nafasi hiyo ambayo pia ilikua ikiwani na nchi nyingine mbili za barani Afrika baada ya kuonekana kwamba fainali hizo za vijana chini ya umri wa miaka 20 haziwezi kufanyika nchini Libya kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo.

Kufuatia hatua ya kuhamishiwa kwa fainali hizo nchini Afrika kusini, timu ya taifa ya nchi hiyo chini ya umri wa miaka 20 imepata nafasi ya kipekee kushiriki baada ya kuenguliwa kwa timu ya taifa ya Libya ambayo haitokua na muda wa kutosha wa kujiandaa.

Fainali hizo zitashuhudia timu nane zilizopangwa kwenye makundi mawili zikiwania nafasi nne za kucheza fainali za kombe la dunia kwa vijana za mwaka huu zitakazofanyika nchini Colombia mwezi June.

Kundi A
Afrika kusini , Mali, Misri pamoja na Lesotho.

Kundi B
Ghana, Nigeria, Cameroon pamoja na Gambia.

CHELSEA, LIVERPOOL ZASHINDA LIGI KUU UINGEREZA.








Chelsea 2-0 Manchester City
Sunderland 0-2 Liverpool.